Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

Kikungwi kufungiwa mita za Tukuza

Jengo la Shiirika la Umeme Zanzibar (ZECO) liliopo Gulioni mjini Zanzibar.

Na Mwashungi Tahir - Maelezo

Shirika la Umeme Zanzibar(ZECO) limesema hadi kufikia mwezi Juni mwakani litakuwa limeshakamilisha zoezi
la ubadilishaji mita za zamani kwa maeneo yote nchini kuwa na mita za tukuza kutokana na kasi ya ufungaji wa mita hizo kufikia hatua ya kuridhisha.

Hayo amesema huko Kikungwi Wilaya ya Kati na Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Salum Abdalla Hassan wakati wa ufungaji wa mita hizo katika eneo hilo, amesema kwa wilaya ya kati ni zaidi ya asilimia tisini 90% zoezi hilo limeshafanyika.

Aidha amewataka wananchi hao kuwa na mwamko wa kutumia huduma za umeme kwani eneo la Kikungwi ni miongoni mwa maeneo yaliyofikishwa huduma ya umeme muda mrefu lakini muitikio wao bado si wa kuridhisha ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina fursa nyingi za kiuchumi.

``Tunawaomba wananchi hasa wa maeneo ya kikungwi wautumie umeme kwa maendeleo kwa sababu kikungwi ni maeneo ya utalii na kutahitajika huduma kubwa za kibiashara ambazo zitahitaji huduma za umeme``, alisema Afisa huyo.

Aidha kwa upande wao wananchi wameelezea matumaini yao kwa kufungiwa mita za tukuza kwani wataondokana na usumbufu pamoja na malalamiko ya mara kwa mara kutokana na mita za zamani.

``Tunaishukuru serikali kwa kutufikishia huduma hii ambayo imetupunguzia masafa na tunaamini huduma hii italeta unafuu na itaondoa ugomvi baina yetu na msomaji mita``,walisema wakazi hao..

Habari