Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

Zanzibar yapigana Vita vifupi zaidi Duniani

Jumba la Kifalme liliopigwa mizinga na Waingereza katika vita vifupi zaidi kutokea.

Na Mwandishi Wetu

Miaka 123 iliyopita, kulizuka vita baina ya Mtawala wa Kisultan wa Zanzibar na Uingereza. Katika kitabu cha matukio muhimu ya Dunia na yaliyovunja rekodi, “The Anglo-Zanzibar war” , ilikuwa vita kati ya Zanzibar na Uingereza iliyotokea Ijumaa ya tarehe 27 August 1896.

Hii ndio vita iliyodumu kwa muda mfupi zaidi hapa duniani, vita ilidumu kwa muda wa dakika arobaini na tano, 45 inagawa machapisho mengine yanasema vita ilidumu kwa muda wa dakika 38, au 40.

Vita ilianza baada ya kifo cha Sultani Hamad bin Thuwaini aliyekuwa mshirika wa utawala wa kikoloni wa waingereza kilichotokea 25.08.1896. Baada ya kifo cha Sultani, 'mpwa' wa Sultani aliyeitwa Khalid bin Bargash (29) alitwaa madaraka, kitu kilichotafsiriwa kama mapinduzi ya kiutawala kwani wakoloni walipendekeza Hamud bin Muhammed awe Sultani ili iwe rahisi kushirikiana naye.

Serikali ya kikoloni ilimtaka Khalid aachie madaraka lakini alikataa na alijiwekea ulinzi wa kijeshi kuzunguka makazi yake ya kisultani.Kufuatia ubishi wa Khalid, wakoloni walikusanya meli tano za kivita baharini karibu na makazi ya Bargash.

Pia waingereza walitoa msaada kwa watu waliokuwa watiifu kwa utawala wa kikoloni ili kupigana dhidi ya Khalid. Dakika za mwishoni kabla ya kuanza kwa vita.

Sultan Khalid alijitahidi kufanya mazungumzo na waingereza kupitia kwa wawakilishi wa Marekani visiwani Zanzibar, lakini jitihada zake hazikufua dafu kwani saa tatu asubuhi ya tarehe 27.08.1896 waingereza walianzisha mashambulizi.

Khalid na jeshi lake hawakuweza kustahimili vishindo vya waingereza kwani walisarenda baada ya dakika 45 za mapigano.

Khalid alitoroka kwenda kwenye 'ubalozi' wa kijerumani, waingereza waliwataka wajerumani wamrejeshe Khalid, lakini haikutokea kwani Oktoba 2, Khalid alitorokea baharini kwenda Dar es Salaam.

Khalid aliishi uhamishoni Dar es Salaam hadi alipokamatwa na waingereza mwaka 1916. Baada ya kukamatwa Khalid aliruhusiwa kuishi Mombasa hadi alipofariki mwaka 1927..

Dunia yetu