Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

JUWAZA yatoa taarifa maadhisho ya Siku ya Wazee Duniani

Katibu wa Jumuiya ya Wazee ya Zanzibar (JUWAZA 2)Aman Suleiman Kombo akitoa taarifa huko Ofisini Kwake Mikunguni kuhusu maadhimisho ya siku ya wazee Duniani yatakayofanyika mwezi ujao huko Kisiwani Pemba kulia ni Naibu Katibu Kombo Mohd Khamis (picha na Kijakazi Abdalla Maelezo)

Na Khadija Khamis, Maelezo

6\09\2019

JAMII imehimizwa kutambua wajibu wa kuwaenzi wazee pamoja na kuthamini mchango walioutoa katika ujenzi wa taifa na kuleta maendeleo nchini.

Katibu wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA 2) Amani Suleiman Kombo, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya wazee duniani yanayotarajiwa kufanyika kitaifa Oktoba 1, 2019 kisiwani Pemba, amesema bila mchango wa wazee maendeleo yanayoonekana sasa yasingekuwepo.

Akizungumza katika ofisi ya jumuiya hiyo Mikunguni mjini Zanzibar, amesema jamii inapaswa kuwapa wazee heshima wanayostahili na sio kuwasharau.

Aidha amekemea vitendo vya udhalilishaji ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakiwafanyia wazee ikiwa ni pamoja na kuwaua, kuwabaka na kuwahusisha na ushirikina.

Katibu huyo alisema wazee ni nguzo muhimu katika kuhakikisha watoto ambao ndio tegemeo la taifa siku za baadae wanapata malezi bora ili wawe wazalendo na msingi wa maendeleo.

Kwa upande mwengine, Amani ameiomba Wizara ya Afya kuweka daktari maalumu katika kila kituo cha afya ambaye ni mtaalamu wa matatizo yanayowakabili wazee ili kuwaepushia usumbufu wanapofika vituoni humo.

Nae Naibu Katibu wa JUWAZA 2 Kombo Mohammed Khamis, amewaomba viongozi wa majimbo kushirikiana na jumuiya za wazee nchini kwa lengo la kuwasaidia wazee walio wagonjwa kupata matibabu.

Aidha aliwataka vijana kuwapa ushirikiano wazee ikizingatiwa kutumia nguvu na maarifa makubwa katika kulipigania taifa.

Mapema, Mlezi wa JUWAZA 2 Hashim Kombo Khamis, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua ya kuwapatia wazee pensheni kila mwisho wa mwezi.

.

Habari