Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

The East African Melody-Homa ya jiji

Kikundi cha East African Melody

Na Dkt Juma Mohammed, MAELEZO

Sanaa ya muziki ni moja ya sekta ambayo inatoa ajira kwa vijana wengi hapa Zanzibar, Tanzania na katika nchi nyengine. Tumeshuhudia sanaa ya muziki ikiwaunganisha watu wa Mataifa mbalimbali na kujiona kuwa ni watu wa familia moja imetoa mchango mkubwa katika jamii.

Ni sanaa ya muziki iliyokuwa ikiwakutanisha wapigania uhuru ambao walitumia muziki kueneza madai ya haki na kutaka Afrika na makoloni mengine yaliyokuwa yakikaliwa na walowezi kutoa uhuru.

Sanaa ya Muziki ilitumika kama silaha ya kuleta mageuzi pale penye dhulma kuhimiza haki na sehemu nyengine muziki uliendelea kufanyakazi ya kuburudisha. Si dhamira ya makala haya leo kuzungumzia mchango wa muziki katika harakati za kupigania ukombozi wa Bara la Afrika, la hasha.

Katika makala haya nitazungumzia mchango wa bendi ya muziki wa Taraab ya The East African Melody ya Zanzibar al maarufu Homa ya Jiji kama ilivyokuwa ikijulikana kwa wakati huo.

Mageuzi yaliyofanywa katika sanaa ya muziki wa taarab hususan ujio wa aina mpya ya taarab inayoitwa ‘Rushwa roho’ ,The East African Melody ni sehemu ya mafanikio ya muziki huo hapa Tanzania.

The East African Melody ilikuwa sio tu ni bendi ya muziki wa taarab,lakini pia ilikuwa ni chuo ambacho kiliwaandaa wasanii katika kada tafauti, utunzi wa nyimbo,utumiaji vyombo, uimbaji, lakini pia iliitangaza Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika anga za kimataifa.

Melody,haikupiga muziki katika viunga vya Zanzibar tu,bali ilitembea mataifa ya Ulaya,Marekani, Arabuni ambako huko watu walizipenda nyimbo za kundi hilo ambalo sasa maskani yake yapo Jijini Dar es Salaam.

Siku hizo, kike kiume hapa Zanzibar ilikuwa huna vya kumwambia lazima siku za ijumaa watu watakwenda kwenye muziki wa homa ya Jiji. Pale mtaani petu Kindongochekundu,kulikua na jirani yetu yeye hakuwa mtu wa kuikosa ‘Homa ya Jiji’ tena alikuwa akishiriki ‘mtambaji bora wa Melody pale ukumbi wa Salama katika hoteli ya Bwawani.

Naweza kusema kwamba East AfricanMelody ilikuwa ni chaguo la umma,hali hii ilikuwa katika kila kona ya Zanzibar, ukitaka ugomvi itoke albam mpya na usiende nayo nyumbani, sijui kitakachotokea, lakini kaka yangu, Hashim Salum anafahamu mambo yalivyokuwa siku hizo.

Kwa hakika The East AfricanMelody iliwaweka pamoja Wazanzibari wenye mitazamo na hisia tafauti,wengine walisahau hata misukosuko ya kisiasa iliyokuwepo kwa wakati ule.

Hata katika shughuli rasmi za kiserikali, The East African Melody ilitimiza wajibu wake katika kuwaburudisha wananchi.

The East African Melody waliimba wimbo wa kuwataka wananchi wa Zanzibar kuishi katika zama za maridhiano, kushindana katika hoja na sio vioja wala vurugu.

Wimbo huo uliopewa jina la “Muafaka” ulipigwa karibu kila kona ya viunga vya Zanzibar mara tu baada ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi(CUF) kusaini muafaka uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola, karibu mji wote watu walipiga wimbo huo.

Katika mchakato mzima wa maridhiano ya kisiasa,kumaliza siasa za kushupaliana, kususiana,kubaguana, The East AfricanMelody nao wanaingia katika orodha ya watu walioshiriki kufanikisha siasa tulivu na za maridhiano kupitia muafaka wa Juni 9 mwaka 1999.

Ijapokuwa vilikuwa vikundi vingi vya muziki,lakini ni The EastAfrican Melody waliosimama katika umma kuwataka kuachana na siasa za chuki, haikuwa jambo jepesi kwa kundi hilo kutunga na kupiga wimbo ule na hasa katika joto la siasa za kushupaliana zilivyokuwa siku zile,lakini EastAfrican Melody,walitanguliza uzalendo mbele katika kuona jamii ya Zanzibar inabakia kuwa moja na yenye maelewano.

The East African Melody walitekeleza wajibu wa wasanii katika nchi na kwa kuwa mcheza kwao hutunzwa, tuna kila sababu na hoja ya kuwatunza East African Melody kwa kuwa Serikali ina utaratibu mzuri wa kutambua na kuthamini kazi za kizalendo zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa, basi katika orodha hiyo Melody tutakuwa tumewatendea haki ikiwa watajumuishwa.

Tunakumbuka kuwa hata uimbaji na utunzi wa The East African Melody mara nyingi walikuwa makini katika uteuzi wa maneno na kwa kiasi fulani hapajatokezea mtu siku hizo na pengine hata sasa kushutumu kazi za Melody katika kuheshimu mila na desturi.

The East African Melody ilianzishwa Dubai mwaka 1993 na ilipofika mwaka 1995 ilianza rasmi kuweka maskani yake Zanzibar, ikiwa na miaka 23 tangu kuanzishwa kwake,hatutaweza kuwaweka katika kaburi la sahau wamiliki wa bendi,marehemu Haji Mohamemed aliekuwa Mkurugenzi,Adam Mlamali, Lamania Shaaban na Mahmoud Alawi.

Kwangu mimi Haji alikuwa ni miongoni mwa watu wangu wa karibu, ni pigo katika ulimwengu wa tasnia ya muziki wa taarab na hususan EastAfrican Melody,nakumbuka wakati fulani nilipokuwa Dar es Salaam mara nyingi tulikuwa tukizungumza na Haji pale Travertine Magomeni.

Haji alinikutanisha na wasanii wengi wa The East African Melody, nilipokuwa nikiandika habari za michezo katika gazeti la Bingwa na Dimba ,Haji Mohammed hakuwa mchoyo wa habari mara zote .

Mila zetu