Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

Siti Binti Saad, Mwanamke wa chuma

Siti Binti Saad

Na Mshenga Hussein

Shekh Shaaban Bin Robert si jina geni hata kidogo masikioni mwa wana Afrika ya Mashariki na wapenzi wa lugha aushi ya Kiswahili. Pia si jina mutashabihati kwa wasomi wa kazi za fasihi ya Kiswahili popote ulimwenguni. Kuna baadhi humuita nguli, shekh (kifani) au baba wa fasihi andishi ya kitanzania. Mie namuita mama wa fasihi! Mama…..? Ndio, MAMA WA FASIHI YA KISWAHILI.

Suala la awaje mama angali ni mwanamume huu sio wakati wake; na wala nisingependa kuutumia wino wangu kuhangaika na hoja dhaifu ya kijinsia au kimfumo dume kama hiyo.

Shaaban Robert amepata kuandika vitabu vingi sana vya Kiswahili ambavyo vina tenzize, nudhumuze, na riwayaze. Yasemwa amepata kuandika zaidi ya vitabu ishirini vya fasihi!

Miongoni mwa vitabu vya Shekh Shaaban bin Robert kipo kitabu kiitwacho “Wasifu wa Siti binti Saad.” Kijitabu hiki ni mkono wa Shaaban Bin Robert katika kupigania ukombozi wa Mwanamke.

Kuna baadhi wanadhani bin Robert ameandika kitabu hiki kwa kubuni wahusika na madhari kama afanyavyo kwenye kazi zake nyingi, mathalan “Kufikirika” na “Kusadikika”, Hasha!

Kitabu hiki si chakubuni hata kidogo bali ni wasifu wa kweli wa mwanamuziki hodari na Baba wa tarabu ya Afrika Mashariki, hee..!

Awaje baba SITI BINTI SAAD? Mie sio mtaalam wa viumbe kusema nimeandika kuchambua masuala ya jinsia katika andiko la kimapambano kama hili. Hivyo siwezi kujibu hoja dhaifu namna hiyo ambayo ni zao la uvivu wa kufikiri. “Asiyefikiri akokotwe kama mkokoteni”.

Shaaban Bin robert hakupenda kuiachia Dunia maarifa mengi ya kimaadili tu bali pia aliitumia kalamu yake kuelezea mapambano halisi ya kitabaka na kimapinduzi.

Wasomi wa kazi za bin Robert wakivua mawani zao za mbao watayaona mengi mno ambayo Shekh hakutaka yabaki tu vitabuni kwa kivuli cha ufasihi bali yawekwe vitendoni haswa, kwani fasihi ni zao la jamii yenye kulenga kuikomboa jamii. Na ndio sababu akatuandikia wasifu wa mwanamke shupavu wa fikira na mtanashati wa sauti na libasi, SITI BINTI SAAD.

Shaaban Bin Robert ameandika kijitabu hiki cha wasifu wa Siti binti Saad kama silaha ya mwanamke katika kujikomboa toka kwenye makucha ya mfumo dume ambao kwa miaka yote umekua dubwana likanyagalo haki na maendeleo ya kweli ya mwanamke katika jamii.

Katika mapambano hayo bin Robert anaonesha kuwa mwanamke ni mtu anaetakiwa kukomboka. Ukombozi wa mwanamke ameuangalia kwa macho mawili mapana na angavu sana.

Mosi, ni kujikomboa mwenyewe.

Siti binti saad alikua msichana mzaliwa wa kijiji cha Fumba huko Unguja. Binti huyu hakuwahi kupata elimu ya shule wala chuo ila alipata elimu ya malezi toka kwa wazazi wake masikini; baba mkulima na mama mfinyanzi.

Siti hakujua kusoma wala kuandika kwa maisha yake yote. Siti hakua mzuri wa sura wala umbo la nje, alikulia katika maisha ya umasikini wa kutupwa! Aliishi kwa nyungu: kufinyanga nyungu na kutembea maili nyingi kwa mguu kwenda mjini Unguja kuuza vyungu alivyofinyanga mwenyewe.

Ila katika kujikomboa siti alikaa na kujisaili vizuri alimuradi atambue kilichomo ndani yake kinachoweza kumtoa alipo na kumpeleka daraja jengine la juu. Akagundua kipawa kikwabwa cha sauti alicho jaaliwa na Muumba. Hapo ndipo ALIPOHAMA FUMBA NA KWENDA MJINI UNGUJA.

Kwa hiyari yake aliamua kwenda mjini na kuanza kutafuta walimu wa kumfundisha na kuilea sauti yake ili aweze kuitumia kwenye kuimba. Baada ya meeengi katika mapito, Siti alifanikiwa kuwa mwimbaji mashuhuri Afrika Mashariki nzima na Duniani kote.

SILAHA aliyotumia kujikomboa ni SAUTI. Bin Robert anasema, “Siti alikua si mmoja wa wahuni waliozoea kutoroka kwao wakakimbilia katika miji kukaa kama chaza juu ya mwamba, au kama kupe juu ya mkia wa ng’ombe….. Alikuja mjini kwa kusudi maalum. Alitamani kufanya kazi pale”.

Hakuna sehemu iliposemwa kuwa labda Siti aliitwa mjini; bali alijitoa kwenda kuhangaikia hatma yake mwenyewe. Hakuamini katika imani hafifu na ya kichefuchefu yakuwa “wanawake tukiwezeshwa tunaweza”; nani awawezeshe?

Mwanamke huyu mwenye adili kubwa alipata mafanikio yaliyoiacha Afrika Mashariki mdomo wazi na leo anatajwa kuwa ndie mwasisi wa taarabu ya Kiswahili.

Pili, kukombolewa.

Haya ni mawazo ya kimapinduzi ya Shaaban bin Robert juu ya ukombozi wa mwanamke. Yeye anaona pia kuna haja ya jamii kumkomboa mwanamke.

Anasema “basi ilikua wajibu wa kila nchi kuandaa wanawake wake kwa mapigano yao, kufaulu kwao ndio kushindwa kwa watu wote, umati wa wanawake wa kazi na matendo mbalimbali kama siti ilikua ndilo jeshi lililotakiwa katika wokovu wa Maisha ya Afrika mashariki”.

Pia Shaaban Robert anaeleza wazi kuwa “mwanamke alikua na haki ya kupata nafasi kama ile ya mwanaume katika maendeleo. Ustahili wake wa jambo hili ulikua mkubwa sana, palikua hapana maana wala faida yoyote ya kutoa nafaka kwa mwanaume na kumvi kwa mwanamke, maisha yalikua kama dhamana kubwa kwa mwanaume kama ilivyokuwa kwa mwanamke”.

Pia katika kuandika wasifu huu wa Bibi Siti binti Saad anawafunda wanawake .

Mila zetu