Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

Sheikh Shaaban Robert ‘Shake Spear" wa Afrika’

Sheikh Shaaban Robert.

Na Dkt Juma Mohammed,MAELEZO

Upwa wa Afrika Mashariki utabaki kwenye ramani ya watu wake kupenda utunzi wa vitabu na kazi nyengine za sanaa. Bado jina la mwandishi wa vitabu mashuhuri wa Tanzania,Sheikh Shabaan Robert linagonga vichwa vya wasomi,wanasiasa,wanafunzi na jamii nzima ya watu wa eneo hili na hata katika mataifa mengine.

Pamoja na ukweli huo,lakini bado hakuna juhudi zilizochukuliwa kumuenzi Shakespeare wetu wa Tanzania. Tunakila sababu ya kuwaenzi wazalendo mashuhuri kama Sheikh Shabaan Robert,gwiji wa fasihi ya kiswahili katika upwa wa Afrika Mashariki.

Wakati sasa umefika wa kuthamini kazi zilizofanywa na wasanii wetu wazalendo. Haitoshi kusoma wasifu wa sifa njema makaburini siku ya maziko, inapendeza tukiwathamini watu waliotoa mchango wakati wa uhai wao.

Wale waliotangulia mbele ya haki, hatuna budi kuwaombea dua njema, kuwaenzi,kuwakumbuka kwa kuendeleza yale waliyoyafanya, waliyoanzisha kwa maslahi ya umma.

Imekuwa mazowea kusikia sifa wakipewa wanasiasa tu huku watu wengine wakionekana nafasi yao kuwa haba katika kukumbukwa kitaifa. Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein kumpa tuzo ya Mapinduzi, Mwanamuziki Marijani Rajabu.

Wakati Waingereza wao wakimuenzi "Shake Spear" kutokana na uandishi wake wa vitabu vya fasihi andishi,Tanzania yaonekana wazi kumpa kisogo na kumuweka kando muandishi wake gwiji marehemu Sheikh Shabaan Robert katika kumuenzi na kumthamini.

Shabaan Robert alitoa mchango stahiki katika harakati za mapambano ya uhuru wa Tanganyika. Ni ukweli usiobishiwa kuwa hukuna jambo ambalo katika maisha ya jamii yetu unaloweza kulizungumzia leo hii ambalo hakupata kuliandika na kuligusia.

Alikuwa ni mshairi mahiri ambae mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa kwani kazi zake zinaheshimika katika fasahi ya Kiswahili na pia zinatumika mashuleni. Kwa hakika almarhum Sheikh Shabaan Robert aliandika jumla ya vitabu vipatavyo ishirini na mbili.

Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na Adili na Nduguze, Kusadikika,Kufikirika,Maisha yangu na baada ya miaka hamsini, Kielelezo cha Fasihi, Mapenzi Bora, Wasifu wa Siti Bint Saad Masomo yenye adili, Utenzi wa Vita vya Uhuru navitaja kwa uchache. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Mataifa mbalimbali.

Marehemu Sheikh Shaaban Robert alizaliwa Januari mosi mwaka 1909 katika Kijiji cha Vimbambani kusini mwa Jiji la Tanga katika upwa wa Afrika Mashariki. Kwasababu ya hali duni ya maisha ya Waafrika wengi na vikwazo vya ukoloni kwa wakati huo, marehemu Sheikh Shaab Robert hakubahatika kupata fursa ya kusoma elimu ya Chuo Kikuu kama ilivyo kwa wengine.

Alisoma katika shule ya Msimbazi, ya Mzizima(sasa Dar-es-salaam) kati ya mwaka 1922 na 1926 alifaulu na kupata cheti. Kazi yake ya kwanza ni ukarani katika Serikali katika Idara ya Forodha Pangani Mkoani Tanga alikoanza mwaka 1926 – 1944.

Kulingana na kumbukumbu inaelezwa kuwa marehemu Sheikh Shaaban Robert alikuwa ni mwanafunzi hodari shuleni na alitokea wa pili katika wanafunzi 11 waliofaulu mitihani yao na kupewa cheti (School Leaving Certificate).

Alioa mara tatu, mke wa kwanza alikuwa Mdigo. Alikuwa na watoto kumi. Alipofariki aliacha watoto watano. Pia aliacha dada yake (wa baba mmoja) Mwana Saumu, na Mama yake.Ni ukweli kwamba kuishi kwake miaka mingi Tanga katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili katika Tanganyika ya kale,kumesaidia maendeleo yake kama mwandishi wa Kiswahili.

Hakuishia kufanyakazi Pangani tu, Mwazuoni huyo pia alifanyakazi katika Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Afisi nyengine.Mbali na kazi yake Fasihi, andishi alikuwa na athari kubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Bodi ya Lugha Tanganyika na nyenginezo.

Kwa hakika , Sheikh Shaaban Robert ni hazina na lulu Tanzania, lakini kwa bahati mbaya sana thamani ya kazi yake imekuwa si lolote si chochote kuanzia kwa Serikali na hata jamii ya Watanzania.

Mhakiki mmoja wa Fasihi, Bitugi Matundura anamuelezea Shaaban Robert kama mtu aliyefanyiwa dhulma situ katika kazi zake,lakini hata katika kumuenzi na ndio maana hivi leo nami naungana na wale wote katika safari hii.

Anakiri Bitugi katika Maelezo yake kuwa tathmini ya jicho kali ya waandishi wa fasihi ya Kiswahili inaonesha kwamba, marehemu Sheikh Shaaban Bin Robert ni miongoni wa watunzi walioacha taathira kubwa mno katika ulingo wa fasihi hiyo.

Anamwelezea Mwandishi huyo kwa uchungu mkubwa huku akifananisha na waandishi wengine wa Afrika waliopuuzwa na Mataifa yao huku wakinakiri hotuba baadhi ya maneno ya waandishi wa kigeni.

Ingawaje alipata sifa kemkem kwa wakati ule na wengine walifikia hadi kumpachika jina la `Shakespeare wa Afrika Mashariki' sifa huwa kwa hakika haziliki.

Lugha ya Kiswahili ni adhim,lulu na johari.Mchango wa mwandishi huyu katika jamii ya watanzania,haukwepeki,hauzuiliki na hautasahaulika.

Safari yake ndefu akitokea Tanga hadi Unguja .

Mila zetu