Untitled Document
home | tume | utangazaaji | znz

SMZ yanunua vifaa vya kisasa vya ujenzi wa barabara




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akitembelea Kituo cha Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara Kibele Wilaya ya Kati Unguja kuangalia Vifaa Vipya vua Ujenzi wa Barabara Zanzibar.(Picha na Maktaba yetu)

Na Dkt Juma Mohammed, MAELEZO

Kwenye nuru hii kuna walio gizani, tena katika giza totoro. Hawana tofauti ya mawazo na wanasiasa wa kale katika zama mpya za kisiasa tulizokuwa nazo ambazo kigezo kimojawapo cha cha kiongozi bora anayewajali wananchi wenzake ni utekelezaji wa ahadi na mipango iliyopangwa.

Jana Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wametembelea kutazama vifaa vipya na vya kisasa vilivyonunuliuwa na SMZ vya kutengenezea barabara ukiwemo mtambo wa lami wa digitali ambavyo hivi sasa vimewekwa Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Hii ni moja kati ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM. Wahenga wanasema haja ya mja kunena, Muungwana vitendo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein anatekeleza falsafa ya kujitegemea.

Umakini , uadilifu, uzalendo na uchapaji kazi uliotukuka wa Rais Dkt Shein leo tunatembea kifua mbele kwa kuwa na vifaa vya kisasa kabisa vya ujenzi wa barabara vikiwa ni mali yetu.

Katika maelezo yake mara baada ya kukagua vifaa hivyo na kupata maelezo kutoka uongozi wa wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dkt. Shein alieleza kuwa ni azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutekeleza ahadi zake za ujenzi wa barabara ambazo iliahidi kwa wananchi.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa ahadi kwa wananchi za ujenzi wa barabara mbali mbali za Unguja na Pemba lakini nyengine zilijengwa na nyengine bado hazijafanyiwa ujenzi kutokana na uhaba na ukosefu wa viifaa vya kutosha vya ujenzi wa barabara.

Vifaa hivyo vimeagizwa kutoka Kampuni zenye sifa kimataifa kutoka nchi za Italia, Brazil, Ujerumani, Japan pamoja na India vimegharimu shilingi bilioni Bilioni 10.3.

Pamoja na jitihada zote hizo, lakini bado kuna wengine wanajifanya hawaoni, hawasikii. Hawa wananikumbusha kisa cha mwanafalsafa wa Ugiriki ya kale,Socrates,ambae siku moja aliamua kutembea viunga vya marikiti mchana kweupe jua la utosi akiwa na kurunzi ikimulika kama vile anaetembea gizani.

Waungwana wakaanza kumshangaa,wale wenzangu na mimi tusioiweza midomo yetu, wakamuuliza. Vipi Sheikh mbona una kurunzi?

Akawajibu kwamba ”Kwenye nuru hii mnayoiona , kuna walio gizani.” Naam, ujio wa vifaa hivi vipya kuna wanaojifanya wako gizani, wakipandisha tanga na kushusha, sijui watafika lini safari ya kutegemea tanga bovu huku kusi anavuma, wengine bado wanashikilia ukale, wanategemea siasa za kusadikika, siasa za porojo, za kuishi kwa matumaini.

Hapa nakumbuka maneno ya Sheikh Shabaan Robert katika ,kitabu chake cha Kielelezo cha Fasahi alisema “Nashikilia ukale kama ni lazima na huuacha vile vile ikiwa haunifai.

Nitaendeleza kubadili mambo kwa sababu siwezi kuwa mtumwa wa kutenda hayo kwa hayo nikazuia bidii yangu. Ukale uniletea mashaka nikajidai kuwa ni wajibu wangu”

Nimekariri matamshi hayo ya Sheikh Shaaban Robert nikinasibisha na matamshi ya wale wanaong’ang’ania ukale kwa kubeza mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 55 chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kitabu cha Cycles of American kilichotungwa na Arthum Schelesinger Jr anasema kutokufungwa na mawazo ya kale katika mazingira yanayobadilika kunampa kiongozi wa kidemokrasia nafasi ya kutengeneza maonjo matamu ili apendwe na kufurahiwa na wengi.

Rais wetu Dkt Shein ni rais wa kidemokrasia na ni miongoni mwa viongozi wasiofungwa na mawazo ya kale. Rais Dkt Shein kila uchao anabadili nchi kufikia katika maendeleo endelevu na hili ndilo jambo ambalo wananchi wanalotaka kufanyiwa na serikali yao na sio porojo za domo mtindi, maziwa kwa mwenye ng’ombe.

Kununuliwa kwa vifaa hivi kuna tosha kumvua chui ngozi ya kondoo, hao hao wanaobeza ndio hao hao na magari yao wanakuwa wa mwanzo kupita katika barabara za lami zilizojengwa na zitakazojengwa kwa fedha za Serikali.

Rais Dkt Shein amewahakikishia wananchi kuwa ahadi zote zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kutengeneza barabara kubwa na ndogo zitatekelezwa baada ya vifaa vipya na vya kisasa kuwasili.

“ Furaha yangu ni kwamba kazi hii itakamilika na hatimae tutajenga wenyewe, kwa fedha zetu wenyewe na wataalamu wetu wenyewe kwa vifaa vyetu wenyewe na kwa nguvu zetu wenyewe kwani azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kufanya hivyo”,Amesema Rais Dkt. Shein.

Ziara ya Mawaziri wa SMZ kujionea wenyewe vifaa hivyo kuna mengi nimejifunza, mosi nami nilikuwa sehemu ya ujumbe uliotembelea huko kibele nimeona kwa macho yangu aina ya vifaa vilivyonunuliwa ambavyo kwa haraka haraka unaweza kudhani kuwa vifaa hivyo vipo katika dunia ya kwanza.

Pili mikakati ya Serikali baada ya kuwasili kwa vifaa hivyo kutaongeza kazi ya utendaji kazi kwa Wizara yenye dhamana ya masuala ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kukamilisha kazi za ujenzi kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.

Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ununuzi wa vifaa hivi bila shaka vitatuweka katika ujenzi wa barabara zetu.

Makala nyingine